Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 15:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Abiya alianza kutawala huko Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu, mwanawe Nebati.

2. Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Absalomu.

3. Abiya alitenda dhambi zilezile alizotenda baba yake, wala hakuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama alivyokuwa babu yake Daudi.

4. Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi-Mungu alimpatia Abiya mwana atakayetawala baada yake, kuwa taa ya kuangaza Yerusalemu na kuuweka imara mji wa Yerusalemu.

5. Mwenyezi-Mungu alifanya hivyo kwa kuwa Daudi alitenda mema mbele yake na hakukiuka aliyomwamuru Mwenyezi-Mungu siku zake zote, isipokuwa tu ule mkasa wa Uria, Mhiti.

6. Kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote alipokuwa mtawala.

7. Matendo mengine ya Abiya, na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Abiya na Yeroboamu waliishi katika hali ya vita.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 15