Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 7:8-17 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Basi, wakamwambia Samueli, “Usiache kumlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu. Endelea kumlilia atuokoe kutoka kwa Wafilisti.”

9. Kwa hiyo Samueli alichukua mwanakondoo anayenyonya akamtolea Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa nzima. Kisha Samueli akamlilia Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Israeli, naye akajibu kilio chake.

10. Samueli alipokuwa anatoa ile sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti walikaribia kuwashambulia Waisraeli. Lakini Mwenyezi-Mungu akatoa sauti kubwa ya ngurumo dhidi ya Wafilisti, na kuwavuruga Wafilisti, nao wakatimuliwa mbele ya Waisraeli.

11. Waisraeli walitoka Mizpa na kuwafuatilia Wafilisti mpaka karibu na mji wa Beth-kari, wakawaangamiza.

12. Kisha, Samueli alichukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mizpa na Sheni, akaliita jiwe hilo Ebenezeri akisema, “Mwenyezi-Mungu ametusaidia mpaka sasa.”

13. Siku hiyo Wafilisti walishindwa; na Mwenyezi-Mungu aliwazuia Wafilisti kuivamia nchi ya Israeli wakati wote Samueli alipokuwa hai.

14. Miji yote ya Waisraeli ambayo Wafilisti waliiteka kati ya Ekroni na Gathi ilirudishiwa Waisraeli, nao walikomboa nchi yao kutoka kwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Waisraeli na Waamori.

15. Samueli alikuwa mwamuzi wa Israeli maisha yake yote.

16. Kila mwaka Samueli alitembelea Betheli, Gilgali na Mizpa, na kuwaamua Waisraeli katika miji hiyo yote.

17. Kisha, alikuwa akirudi Rama, maana huko kulikuwa nyumbani kwake; aliwaamulia Waisraeli haki zao huko, na kumjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 7