Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 25:6-24 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Mtamwambia kwamba Daudi anakusalimu hivi: ‘Amani iwe kwako, kwa jamaa yako na yote uliyo nayo.

7. Nimesikia kwamba unawakata manyoya kondoo wako nataka ujue kwamba wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, nasi hatukuwadhuru. Tena muda wote walipokuwa pamoja nasi mjini Karmeli, hawakukosa chochote.

8. Ukiwauliza, watakuambia. Sasa nakuomba vijana wangu hawa wapate kibali mbele yako, kwani tumefika wakati wa sikukuu. Tafadhali uwapatie chochote ulicho nacho watumishi wako hawa nami mwanao Daudi.’”

9. Wale vijana wa Daudi walikwenda na kumwambia Nabali kama walivyoagizwa na Daudi. Halafu wakasubiri kidogo.

10. Kisha Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaowakimbia mabwana zao.

11. Je, nichukue mikate yangu, maji yangu na nyama niliyowachinjia wakata-manyoya ya kondoo wangu na kuwapa watu ambao sijui hata wanakotoka?”

12. Basi, wale vijana wa Daudi walirudi na kumwambia Daudi walivyojibiwa.

13. Hivyo Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni.” Kila mtu akajifunga upanga wake, na Daudi pia akajifunga upanga wake; watu wapatao 400 wakamfuata Daudi na watu 200 wakabaki na mizigo.

14. Kijana mmoja wa Nabali, akamwambia Abigaili, mkewe Nabali, “Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani ili kumsalimu bwana wetu. Lakini yeye aliwatukana.

15. Lakini watu hao walikuwa wema sana kwetu, hawakutudhuru; na wakati wote tulipokuwa nao huko nyikani hatukukosa chochote.

16. Kwetu, walikuwa kama ukuta wa ulinzi usiku na mchana muda wote tulipokuwa tunawachunga kondoo.

17. Sasa fikiria juu ya jambo hili na uamue la kufanya. Jambo hili laweza kuleta madhara kwa bwana wetu na jamaa yake yote. Yeye ni mtu mbaya na hakuna anayeweza kuzungumza naye.”

18. Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate 200, viriba viwili vya divai, kondoo watano walioandaliwa vizuri, kilo kumi na saba za bisi, vishada 100 vya zabibu kavu, mikate ya tini 200, na vitu hivi vyote akavipakia juu ya punda.

19. Akamwambia yule kijana wake, “Tangulia! Mimi nitakufuata.” Lakini hakumwambia mumewe lolote.

20. Alipokuwa anateremka, amepanda punda wake, na kukingwa na mlima upande mmoja, akakutana kwa ghafla na Daudi na watu wake wakiwa wanaelekea upande anakotoka.

21. Daudi alikuwa akifikiri, “Mimi nimekuwa nikilinda mali yote ya Nabali nyikani bila faida yoyote na hakuna kitu chake chochote kilichopotea, naye amenilipa mabaya kwa mema niliyomtendea.

22. Mungu na aniue mimi ikiwa kesho asubuhi nitakuwa sijawaua wanaume wake wote.”

23. Abigaili alipomwona tu Daudi, akashuka mara moja kutoka juu ya punda wake, na kuinama mbele ya Daudi hadi uso wake ukagusa chini.

24. Alijitupa miguuni pa Daudi na kumwambia, “Bwana wangu, hatia yote na iwe juu yangu tu. Nakuomba niongee nawe mimi mtumishi wako. Nakuomba usikilize maneno ya mtumishi wako.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 25