Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 25:6-17 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Mtamwambia kwamba Daudi anakusalimu hivi: ‘Amani iwe kwako, kwa jamaa yako na yote uliyo nayo.

7. Nimesikia kwamba unawakata manyoya kondoo wako nataka ujue kwamba wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, nasi hatukuwadhuru. Tena muda wote walipokuwa pamoja nasi mjini Karmeli, hawakukosa chochote.

8. Ukiwauliza, watakuambia. Sasa nakuomba vijana wangu hawa wapate kibali mbele yako, kwani tumefika wakati wa sikukuu. Tafadhali uwapatie chochote ulicho nacho watumishi wako hawa nami mwanao Daudi.’”

9. Wale vijana wa Daudi walikwenda na kumwambia Nabali kama walivyoagizwa na Daudi. Halafu wakasubiri kidogo.

10. Kisha Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumishi wengi wanaowakimbia mabwana zao.

11. Je, nichukue mikate yangu, maji yangu na nyama niliyowachinjia wakata-manyoya ya kondoo wangu na kuwapa watu ambao sijui hata wanakotoka?”

12. Basi, wale vijana wa Daudi walirudi na kumwambia Daudi walivyojibiwa.

13. Hivyo Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni.” Kila mtu akajifunga upanga wake, na Daudi pia akajifunga upanga wake; watu wapatao 400 wakamfuata Daudi na watu 200 wakabaki na mizigo.

14. Kijana mmoja wa Nabali, akamwambia Abigaili, mkewe Nabali, “Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani ili kumsalimu bwana wetu. Lakini yeye aliwatukana.

15. Lakini watu hao walikuwa wema sana kwetu, hawakutudhuru; na wakati wote tulipokuwa nao huko nyikani hatukukosa chochote.

16. Kwetu, walikuwa kama ukuta wa ulinzi usiku na mchana muda wote tulipokuwa tunawachunga kondoo.

17. Sasa fikiria juu ya jambo hili na uamue la kufanya. Jambo hili laweza kuleta madhara kwa bwana wetu na jamaa yake yote. Yeye ni mtu mbaya na hakuna anayeweza kuzungumza naye.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 25