Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 12:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Lakini mlipomwona mfalme Nahashi wa Waamoni amekuja kuwashambulia, mkamkataa Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mfalme wenu, mkaniambia, ‘La! Mfalme ndiye atakayetutawala.’

13. Sasa, mfalme mliyejichagulia ndiye huyu hapa. Mlimwomba Mwenyezi-Mungu awape mfalme, naye amewapa.

14. Kama mkimcha Mwenyezi-Mungu, na kumtumikia, na kusikiliza sauti yake bila kuiasi amri yake, kama nyinyi wenyewe pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi mtafanikiwa.

15. Lakini kama hamtasikiliza sauti ya Mwenyezi-Mungu, mkaasi amri yake, basi yeye atapambana nanyi pamoja na mfalme wenu.

16. Kwa hiyo basi, tulieni na kulitazama jambo hilo kubwa ambalo Mwenyezi-Mungu atatenda mbele yenu.

17. Je, sasa si wakati wa kuvuna ngano? Lakini mimi nitamwomba Mwenyezi-Mungu alete radi na mvua, nanyi mtatambua na kuona kuwa uovu wenu mliotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kujitakia mfalme, ni mkubwa.”

18. Basi, Samueli akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akatuma radi na mvua katika siku hiyo. Watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu na Samueli.

19. Hivyo wakamwambia Samueli, “Tafadhali utuombee sisi watumishi wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili tusife; kwa sababu tumezidisha dhambi zetu kwa uovu huo wa kujitakia mfalme.”

20. Samueli akawajibu, “Msiogope; ingawa mmefanya uovu huu, msiache kumfuata Mwenyezi-Mungu, ila mtumikieni kwa moyo wenu wote.

21. Msiifuate miungu ya uongo isiyo na faida wala haiwezi kuwaokoa, maana ni ya uongo.

22. Kwa heshima ya jina lake kuu, Mwenyezi-Mungu hatawatupa watu wake kwa sababu amependa kuwafanya nyinyi muwe watu wake.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 12