Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 29:22-30 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Basi siku hiyo walikula na kunywa kwa furaha kuu mbele ya Mwenyezi-Mungu.Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi, mara ya pili. Wakampaka mafuta awe mtawala kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na Sadoki awe kuhani.

23. Ndipo Solomoni akaketi katika kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu, badala ya Daudi baba yake. Naye akafanikiwa, na taifa lote la Israeli likamtii.

24. Viongozi wote, mashujaa na wana wote wa Daudi wakajiweka chini ya mfalme Solomoni.

25. Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni sifa nzuri machoni pa Waisraeli wote, akampa fahari ya kifalme ipitayo fahari ya mfalme awaye yote aliyeitawala Israeli kabla yake.

26. Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli yote.

27. Na muda aliotawala juu ya Israeli ulikuwa miaka arubaini; miaka saba alitawala huko Hebroni na miaka thelathini na mitatu alitawala huko Yerusalemu.

28. Alikufa akiwa mzee mwenye miaka mingi, ameshiba siku, akiwa na mali na heshima. Solomoni mwanawe, akawa mfalme badala yake.

29. Habari za mfalme Daudi toka mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samueli mwonaji, katika kumbukumbu za nabii Nathani na katika kumbukumbu za Gadi mwonaji.

30. Hizo zasema pamoja na mambo ya utawala wake, uwezo wake, na mambo yaliyompata yeye, Waisraeli, na falme zote nchini.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 29