Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 28:12-21 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Alimpa ramani ya yote aliyokusudia moyoni kuhusu nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, vyumba vya Mungu na ghala za kuwekea vitu vilivyo wakfu.

13. Alimpa pia mfano wa jinsi ya kuwapanga makuhani na Walawi kuzitekeleza huduma zao, kutumikia nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuvitunza vyombo vyote vya Nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

14. Alimpa kiasi cha dhahabu iliyohitajika kutengenezea vyombo vyote vya dhahabu vya utumishi wa kila namna, kiasi cha fedha iliyohitajika kwa utumishi wa kila namna,

15. uzani wa vinara vya dhahabu na taa zake, uzani wa dhahabu ya kila kinara na taa zake uzani wa fedha ya kutengenezea kinara na taa zake kulingana na matumizi ya kila kinara;

16. na kiasi cha dhahabu ya kutengenezea meza za dhahabu zilizowekewa mikate iliyotolewa kwa Mungu, hata kiasi cha fedha ya kutengenezea meza za fedha;

17. pia alitoa maagizo kuhusu kiasi cha dhahabu safi iliyohitajika kutengenezea nyuma, mabirika na vikombe, pia kiasi cha dhahabu na fedha iliyohitajika kutengenezea mabakuli ya dhahabu na ya fedha,

18. na kiasi cha dhahabu safi ya kutengenezea madhabahu ya kufukizia ubani. Alimpa pia mfano wake wa gari la dhahabu la viumbe wenye mabawa waliyotandaza mabawa na kulifunika sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.

19. Hayo yote, mfalme Daudi aliyaweka wazi kwa maandishi aliyopewa na Mwenyezi-Mungu. Kazi yote itendeke kulingana na ramani hiyo.

20. Kisha, mfalme Daudi akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe imara na hodari, uifanye kazi hii. Usiogope wala kuwa na wasiwasi. Mungu, Mwenyezi-Mungu ambaye ni Mungu wangu, yu pamoja nawe. Hatakuacha bali atakuwa nawe hata itakapomalizika kazi yote inayohitajika kufanyiwa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

21. Makuhani na Walawi wamekwisha pangiwa kazi watakazofanya katika nyumba ya Mungu. Wafanyakazi wenye ujuzi wa kila aina watakuwa tayari kabisa kukusaidia, na watu wote pamoja na viongozi wao watakuwa chini ya amri yako.”

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 28