Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 26:12-27 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Mabawabu hao waligawanyika katika makundi kulingana na jamaa zao, nao pia walipangiwa kazi kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama wale Walawi wengine.

13. Kila jamaa, bila kujali wingi, ilipiga kura kuchagua lango watakalosimamia.

14. Kura ya kuchagua wa kulinda lango la mashariki ilimwangukia Shelemia. Walipiga kura pia kwa ajili ya mwanawe Zekaria, aliyekuwa mshauri mwenye busara, ikamwangukia kura ya lango la kaskazini.

15. Obed-edomu aliangukiwa na kura ya lango la kusini, na ya wanawe, ghala.

16. Shupimu na Hosa waliangukiwa na kura ya kulinda lango la magharibi kwenye lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu. Ulinzi ulifanywa kwa zamu.

17. Kila siku upande wa mashariki kulikuwa na mabawabu sita, kaskazini wanne, na kusini wanne, pia kwenye ghala kuliwekwa mabawabu wawiliwawili.

18. Kwenye banda zuri lililokuwa upande wa magharibi, kulikuwa na mabawabu wanne barabarani, na wawili kwenye banda lenyewe.

19. Haya ndiyo makundi ya mabawabu miongoni mwa ukoo wa Kora na wazawa wa Merari waliofanya kazi ya ubawabu.

20. Miongoni mwa Walawi, Ahiya alihusika na uangalizi wa hazina ya nyumba ya Mungu, na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu.

21. Ladani, mmoja wa ukoo wa Gershoni, alikuwa babu wa baadhi ya jamaa, miongoni mwao ikiwamo jamaa ya mwanawe Yehieli.

22. Wana wengine wawili wa Ladani, Zethamu na Yoeli, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

23. Pia kazi ziligawanywa kwa watu wa koo za Wasiria, Waishari, Wahebroni na Wauzieli.

24. Shebueli, mwana wa Gershoni, mwana wa Mose, alikuwa ofisa mkuu wa hazina hizo.

25. Na ndugu yake, alikuwa Eliezeri, aliyekuwa baba yake Rehabia, aliyemzaa Yeshaya, aliyemzaa Yoramu, aliyemzaa Zikri, aliyemzaa Shelomithi.

26. Shelomithi na ndugu zake, ndio waliokuwa waangalizi wa hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu na mfalme Daudi, na viongozi wa jamaa, maofisa wa maelfu na mamia na majemadari wa jeshi.

27. Waliweka wakfu sehemu ya nyara walizoteka vitani kwa ajili ya matengenezo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 26