Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 21:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Hivyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Jichagulie mojawapo:

12. Njaa ya miaka mitatu, au miezi mitatu ya maangamizi kutokana na maadui zako ambapo upanga wa maadui zako utakushinda; au siku tatu ambapo Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa upanga wake, awaletee maradhi mabaya nchini, na malaika wake apite kuwaangamiza katika nchi nzima ya Israeli. Sasa amua, ni jibu lipi nitakalompa yeye aliyenituma.”

13. Daudi akamjibu Gadi, “Nimeingia katika mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu kwani yeye ana huruma sana. Ila nisianguke katika mkono wa mwanadamu.”

14. Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi mabaya, ambayo yalisababisha vifo vya Waisraeli 70,000.

15. Halafu Mungu akatuma malaika aende kuuharibu Yerusalemu; lakini kabla hajafanya hivyo, Mwenyezi-Mungu akageuza nia yake na kumwambia malaika huyo aliyetekeleza maangamizi, “Basi, yatosha!” Malaika alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi.

16. Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama kati ya mbingu na dunia, naye ameunyosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuuangamiza. Hapo Daudi na wazee wote walikuwa wamevaa mavazi ya gunia, wakaanguka kifudifudi.

17. Daudi alimwambia Mungu, “Je, si mimi niliyetoa amri watu wahesabiwe? Ni mimi niliyetenda dhambi na kufanya uovu. Lakini kondoo hawa wamefanya nini? Nakusihi sana, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mkono wako uwe dhidi yangu na dhidi ya jamaa ya baba yangu, lakini maradhi haya mabaya yasiwapate watu wako.”

18. Ndipo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi aende amjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Ornani Myebusi.

19. Daudi akatii amri ya Mwenyezi-Mungu, akapanda juu kufuatana na neno la Gadi alilosema kwa jina la Mwenyezi-Mungu.

20. Ornani alipogeuka na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Ornani alikuwa akipura ngano.

21. Daudi alipomwendea Ornani, Ornani alitazama na kumwona Daudi; basi huyo Ornani alitoka kwenye uwanja wa kupuria akaenda mbele; kisha akamsujudia akiinamisha kichwa chake mpaka chini ardhini.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 21