Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 11:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha Waisraeli wote walikusanyika pamoja kwa Daudi huko Hebroni, wakamwambia: “Tazama, sisi ni mwili na damu yako.

2. Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alikuambia, ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli, na utakuwa mkuu wa watu wangu Israeli.’

3. Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye Daudi akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Waisraeli kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu lililotolewa kwa njia ya Samueli.”

4. Baadaye Daudi na Waisraeli wote walikwenda Yerusalemu uliojulikana kama Yebusi, na ambao wenyeji wake walikuwa Wayebusi.

5. Wakazi wa Yebusi walimwambia Daudi, “Hutaingia katika mji huu.” Hata hivyo, Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi.

6. Ndipo Daudi akasema, “Mtu atakayetangulia kuwapiga Wayebusi, atakuwa mkuu na kamanda jeshini.” Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akawa wa kwanza kuwashambulia, hivyo akawa mkuu.

7. Daudi alikaa katika ngome hiyo, na kwa hiyo, mji huo ukaitwa “Mji wa Daudi.”

8. Aliujenga mji huo, akianzia Milo, na kuuzunguka wote, na Yoabu akautengeneza mji huo upya.

9. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu kwa sababu Mwenyezi-Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye.

10. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli.

11. Ifuatayo ni orodha ya mashujaa hao wa Daudi: Yashobeamu, Mhakmoni, aliyekuwa kiongozi wa “Wale thelathini.” Yeye alipigana kwa mkuki wake akaua watu 300 kwa mara moja vitani.

12. Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, Mwahohi.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 11