Agano la Kale

Agano Jipya

Yuda 1:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu

15. kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”

16. Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe.

17. Lakini nyinyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo.

18. Waliwaambieni: “Siku za mwisho, watatokea watu watakaowadhihaki nyinyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.”

19. Hao ndio wanaosababisha mafarakano, watu wa fikira za kidunia, wasio na Roho wa Mungu.

20. Lakini nyinyi, wapenzi wangu, jijengeni wenyewe juu ya imani yenu takatifu kabisa. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,

21. na kudumu katika upendo wa Mungu, mkimngojea Bwana wetu Yesu Kristo ambaye, kwa huruma yake, atawajalieni uhai wa milele.

22. Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka;

23. waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni. Lakini kwa wengine muwe na huruma pamoja na tahadhari, mkichukia hata mavazi yao yenye madoa ya tamaa zao mbaya.

24. Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake,

25. kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.

Kusoma sura kamili Yuda 1