Agano la Kale

Agano Jipya

Yohane 8:38-51 Biblia Habari Njema (BHN)

38. Mimi nasema yale aliyonionesha Baba, lakini nyinyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”

39. Wao wakamjibu, “Sisi ni watoto wa Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama nyinyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu.

40. Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, nyinyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!

41. Nyinyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya baba yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.”

42. Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.

43. Kwa nini hamuelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.

44. Nyinyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.

45. Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana nyinyi hamniamini.

46. Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?

47. Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini nyinyi hamsikilizi kwa sababu nyinyi si watu wa Mungu.”

48. Wayahudi wakamwambia, “Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?”

49. Yesu akajibu, “Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini nyinyi hamniheshimu.

50. Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.

51. Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele.”

Kusoma sura kamili Yohane 8