Agano la Kale

Agano Jipya

Yohane 4:27-40 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?”

28. Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,

29. “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?”

30. Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.

31. Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, kula chakula.”

32. Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua nyinyi.”

33. Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?”

34. Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.

35. Nyinyi mwasema: ‘Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!’ Lakini mimi nawaambieni, angalieni mkaone jinsi mashamba yalivyo tayari kuvunwa.

36. Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uhai wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.

37. Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna.’

38. Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho; wengine walifanya kazi, lakini nyinyi mnafaidika kutokana na jasho lao.”

39. Wasamaria wengi wa kijiji kile walimwamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.”

40. Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili.

Kusoma sura kamili Yohane 4