Agano la Kale

Agano Jipya

Yakobo 5:4-16 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi.

5. Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa.

6. Mmemhukumu na kumuua mtu asiye na hatia, naye hakuwapingeni!

7. Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno ya thamani. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli.

8. Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia.

9. Ndugu zangu, msinung'unikiane nyinyi kwa nyinyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia.

10. Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana.

11. Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema.

12. Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni “Ndiyo” kama maana yenu ni ndiyo, na “La” kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu.

13. Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa.

14. Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.

15. Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa.

16. Basi, ungamanieni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi.

Kusoma sura kamili Yakobo 5