Agano la Kale

Agano Jipya

Yakobo 2:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Kama mnaitimiza ile sheria ya ufalme kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”, mtakuwa mnafanya vema kabisa.

9. Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo sheria inawahukumu nyinyi kuwa mna hatia.

10. Anayevunja amri mojawapo ya sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja sheria yote.

11. Maana yuleyule aliyesema: “Usizini,” alisema pia “Usiue.” Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini, lakini umeua, wewe umeivunja sheria.

12. Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.

13. Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.

14. Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?

15. Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula.

16. Yafaa kitu gani nyinyi kuwaambia hao: “Nendeni salama mkaote moto na kushiba,” bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?

17. Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.

18. Lakini mtu anaweza kusema: “Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!” Haya! Nioneshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo yangu.

Kusoma sura kamili Yakobo 2