Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 9:19-33 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Labda utaniuliza: “Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?”

20. Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: “Kwa nini umenitengeneza namna hii?”

21. Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida.

22. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake. Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa.

23. Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake.

24. Maana sisi ndio hao aliowaita, si kutoka miongoni mwa Wayahudi tu bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine.

25. Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea:“Wale waliokuwa ‘Si watu wangu’nitawaita: ‘Watu wangu!’Naye ‘Sikupendi’ataitwa: ‘Mpenzi wangu!’

26. Na pale walipoambiwa:‘Nyinyi si wangu’hapo wataitwa:‘Watoto wa Mungu aliye hai.’”

27. Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaza sauti: “Hata kama wazawa wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa;

28. maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote.”

29. Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: “Bwana wa majeshi asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa kama Gomora.”

30. Basi tuseme nini? Watu wa mataifa ambao hawakutafuta wafanywe waadilifu, wamejaliwa kuwa waadilifu, kwa njia ya imani,

31. hali watu wa Israeli ambao walitafuta sheria ya kuwafanya kuwa waadilifu, hawakuipata.

32. Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa

33. kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:“Tazama, nitaweka huko Siyoni jiwe likwazalo,mwamba utakaowafanya watu waanguke.Lakini atakayemwamini hataaibishwa!”

Kusoma sura kamili Waroma 9