Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 8:19-30 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake.

20. Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini,

21. maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu.

22. Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto.

23. Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe.

24. Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona?

25. Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu.

26. Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka.

27. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.

28. Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.

29. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

30. Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.

Kusoma sura kamili Waroma 8