Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 7:9-21 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka,

10. nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo.

11. Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua.

12. Basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri.

13. Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Ilivyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno.

14. Tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi.

15. Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachokichukia ndicho nikifanyacho.

16. Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile sheria ni nzuri.

17. Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi inayokaa ndani yangu.

18. Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza.

19. Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka.

20. Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.

21. Basi, nimegundua kanuni hii: Ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua.

Kusoma sura kamili Waroma 7