Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 5:17-21 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja, kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kufanywa kuwa waadilifu, watatawala katika uhai kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo.

18. Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kiadilifu cha mtu mmoja kinawapa wote uadilifu na uhai.

19. Na kama kwa kutokutii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi kuwa waadilifu.

20. Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi.

21. Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa uadilifu na kuleta uhai wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Kusoma sura kamili Waroma 5