Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 2:4-18 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?

5. Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajirundikia adhabu kwa siku ile ya ghadhabu wakati hukumu ya haki ya Mungu itakapodhihirishwa.

6. Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake.

7. Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele.

8. Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.

9. Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza na watu wa mataifa mengine pia.

10. Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.

11. Maana Mungu hambagui mtu yeyote.

12. Wale wanaotenda dhambi bila kuijua sheria wataangamia ingawaje hawaijui sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua sheria watahukumiwa kisheria.

13. Maana sio wanaosikia sheria ndio walio waadilifu mbele ya Mungu, ila wenye kuitii sheria ndio watakaokubaliwa kuwa waadilifu.

14. Mathalani: Watu wa mataifa mengine hawana sheria; lakini kila wanapotimiza matakwa ya sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha sheria ingawa hawaijui sheria.

15. Mwenendo wao unaonesha kwamba matakwa ya sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea.

16. Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.

17. Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia sheria na kujivunia kuwa wa Mungu;

18. kwa njia ya sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema;

Kusoma sura kamili Waroma 2