Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 11:5-24 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: Ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake.

6. Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena.

7. Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa,

8. kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:“Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito,na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yaowala kusikia kwa masikio yao.”

9. Naye Daudi anasema:“Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa,waanguke na kuadhibiwa.

10. Macho yao yatiwe gizawasiweze kuona.Migongo yao ipindike kwa taabu daima!”

11. Basi, nauliza: Je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu.

12. Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao wa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri kwamba kuingizwa kwa idadi yao kamili kutakuwa ni baraka zaidi.

13. Basi, sasa nawaambieni nyinyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu,

14. nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee nyinyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao.

15. Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka!

16. Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia.

17. Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Nyinyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini.

18. Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si nyinyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza nyinyi.

19. Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.”

20. Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari.

21. Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe?

22. Ona, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa.

23. Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.

24. Nyinyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao.

Kusoma sura kamili Waroma 11