Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 11:13-33 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, sasa nawaambieni nyinyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu,

14. nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee nyinyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao.

15. Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka!

16. Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia.

17. Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Nyinyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini.

18. Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si nyinyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza nyinyi.

19. Lakini utasema: “Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake.”

20. Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari.

21. Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe?

22. Ona, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa.

23. Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.

24. Nyinyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao.

25. Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu.

26. Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:“Mkombozi atakuja kutoka Siyoni,atauondoa uovu wa wazawa wa Yakobo.

27. Hili ndilo agano nitakalofanya naowakati nitakapoziondoa dhambi zao.”

28. Kwa sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa maadui wa Mungu, lakini kwa faida yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni marafiki wa Mungu kwa sababu ya babu zao.

29. Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo.

30. Hapo awali nyinyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na kuasi kwao.

31. Hali kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa nyinyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu.

32. Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili apate kuwahurumia wote.

33. Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:

Kusoma sura kamili Waroma 11