Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 5:17-26 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe.

18. Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya sheria.

19. Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: Uzinzi, uasherati, ufisadi;

20. kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano;

21. husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: Watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao.

22. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,

23. upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo.

24. Wale walio na Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.

25. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.

26. Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.

Kusoma sura kamili Wagalatia 5