Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 5:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa.

2. Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote.

3. Nasema tena wazi: Kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika sheria yote.

4. Kama mnatazamia kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu.

5. Kwa upande wetu, lakini, sisi tunangojea kwa matumaini kwa nguvu ya Roho tufanywe waadilifu kwa njia ya imani.

6. Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo.

7. Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli?

8. Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni.

9. “Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!”

10. Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni – awe nani au nani – hakika ataadhibiwa.

11. Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote.

12. Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe!

13. Nyinyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo.

Kusoma sura kamili Wagalatia 5