Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 4:19-31 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Watoto wangu, kama vile mama mjamzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu.

20. Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi!

21. Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo sheria?

22. Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: Mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru.

23. Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.

24. Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani.

25. Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake.

26. Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu.

27. Maana imeandikwa:“Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa;paza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto;maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengikuliko wa yule aliye na mume.”

28. Sasa, basi, ndugu zangu, nyinyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka.

29. Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi.

30. Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: “Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru.”

31. Hivyo basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.

Kusoma sura kamili Wagalatia 4