Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 3:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaroga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu.

2. Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Injili?

3. Je, nyinyi ni wajinga kiasi hicho? Nyinyi mlianza yote kwa msaada wa Roho, je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe?

4. Je, mambo yale yote yaliyowapata nyinyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani!

5. Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Injili na kuiamini?

6. Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: Yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.

7. Sasa basi, jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu.

8. Maandiko Matakatifu yalionesha kabla kwamba Mungu atawafanya watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: “Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa.”

9. Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini.

10. Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria, yuko chini ya laana.”

11. Ni dhahiri kwamba sheria haiwezi kumfanya mtu kuwa mwadilifu; maana Maandiko yasema: “Mwadilifu kwa imani ataishi.”

12. Lakini sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: “Mwenye kutimiza yanayotakiwa na sheria ataishi.”

Kusoma sura kamili Wagalatia 3