Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 1:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mimi Paulo niliye mtume si kwa mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu,

2. na ndugu wote walio pamoja nami tunayasalimu makanisa ya Galatia.

3. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

4. Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa.

5. Kwake yeye uwe utukufu milele na milele! Amina.

6. Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi Mungu aliyewaita kwa neema ya Kristo, na mnafuata injili ya namna nyingine.

7. Lakini hakuna injili nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo.

8. Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni injili tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe!

9. Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: Kama mtu yeyote anawahubirieni injili ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe!

10. Sasa nataka kibali cha nani: Cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo.

11. Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Injili niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu.

12. Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia.

Kusoma sura kamili Wagalatia 1