Agano la Kale

Agano Jipya

Wafilipi 3:8-17 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo

9. na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani.

10. Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake,

11. nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu.

12. Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi.

13. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele.

14. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu.

15. Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo.

16. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa.

17. Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo.

Kusoma sura kamili Wafilipi 3