Agano la Kale

Agano Jipya

Wafilipi 2:6-21 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Yeye, kwa asili alikuwa daima Mungu;lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Munguni kitu cha kungangania kwa nguvu.

7. Bali, kwa hiari yake mwenyewe,aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi,akawa sawa na wanadamu,akaonekana kama wanadamu.

8. Alijinyenyekesha na kutii mpaka kufa,hata kufa msalabani.

9. Kwa sababu hiyo Mungu alimkweza juu kabisa,akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.

10. Ili kwa heshima ya jina la Yesu,viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,vipige magoti mbele yake,

11. na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana,kwa utukufu wa Mungu Baba.

12. Wapenzi wangu, nilipokuwa nanyi mlinitii daima, na hata sasa niwapo mbali nanyi endeleeni kutii. Fanyeni kazi kwa hofu na tetemeko kwa ajili ya ukombozi wenu,

13. kwani Mungu ndiye afanyaye kazi daima ndani yenu, na kuwapeni uwezo wa kutaka na kutekeleza mambo yanayopatana na mpango wake mwenyewe.

14. Fanyeni kila kitu bila kunungunika na bila ubishi,

15. ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtangara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga,

16. mkishika imara ujumbe wa uhai. Na hapo ndipo nami nitakapokuwa na sababu ya kujivunia katika siku ile ya Kristo, kwani itaonekana dhahiri kwamba bidii yangu na kazi yangu havikupotea bure.

17. Hata ikiwa nitatolewa mhanga pamoja na imani yenu iliyo tambiko kwa Mungu, basi, nafurahi sana na kuwashirikisha nyinyi nyote furaha hiyo.

18. Hali kadhalika nanyi mnapaswa kufurahi na kunishirikisha mimi furaha yenu.

19. Katika kuungana na Bwana Yesu ninalo tumaini kwamba nitaweza kumtuma Timotheo kwenu hivi karibuni, ili nitiwe moyo kwa kupata habari zenu.

20. Sina mtu mwingine kama yeye ambaye anawashughulikieni kwa moyo.

21. Wengine wanashughulikia tu mambo yao wenyewe badala ya kuyashughulikia mambo ya Yesu Kristo.

Kusoma sura kamili Wafilipi 2