Agano la Kale

Agano Jipya

Wafilipi 1:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mimi Paulo na Timotheo, watumishi wa Yesu Kristo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Filipi ambao mmeunganishwa na Kristo Yesu, pamoja na viongozi na wasaidizi wa kanisa.

2. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

3. Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbukeni;

4. na kila ninapowaombeeni nyote, nasali kwa furaha,

5. kwa sababu ya jinsi mlivyonisaidia katika kazi ya Injili tangu siku ile ya kwanza mpaka leo.

6. Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu.

7. Hivyo ndivyo ninavyopaswa kuwafikirieni, kwani nawakumbukeni daima moyoni mwangu. Kwa maana nyinyi nyote mmeshiriki katika fadhili aliyonijalia Mungu ya kutetea na kuithibitisha Injili, sasa niwapo kifungoni na pia pale awali nilipokuwa huru.

8. Mungu anajua kuwa ninasema ukweli ninaposisitiza kwamba, kwa upendo uleule wa Yesu Kristo, natamani sana kuwaoneni.

Kusoma sura kamili Wafilipi 1