Agano la Kale

Agano Jipya

Waebrania 12:22-29 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Lakini nyinyi mmefika katika mlima wa Siyoni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika kwa maelfu.

23. Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa wakamilifu.

24. Mmefika kwa Yesu ambaye ni mpatanishi katika agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema kuliko ile ya Abeli.

25. Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza huyo anayesema nanyi. Kama wale waliokataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni?

26. Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: “Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu.”

27. Neno hili: “Tena” linatuonesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa.

28. Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;

29. maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.

Kusoma sura kamili Waebrania 12