Agano la Kale

Agano Jipya

Ufunuo 19:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu wengi mbinguni ikisema, “Asifiwe Mungu! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!

2. Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!”

3. Wakasema, “Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo utapanda juu milele na milele!”

4. Na wale wazee ishirini na wanne, na wale viumbe hai wanne, wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi wakisema, “Amina! Asifiwe Mungu!”

5. Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.”

6. Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala!

7. Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari.

8. Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watakatifu).

9. Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu.”

10. Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.”

11. Kisha, nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi mmoja mweupe, na mpandafarasi wake aliitwa “Mwaminifu” na “Kweli”. Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki.

12. Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa tu yeye mwenyewe.

13. Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina lake huyo ni “Neno la Mungu”.

14. Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na yamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi.

Kusoma sura kamili Ufunuo 19