Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 28:7-20 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka kwa wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni.”

8. Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake.

9. Mara, Yesu akakutana nao, akasema: “Salamu.” Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake.

10. Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona.”

11. Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia.

12. Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha

13. wakisema, “Nyinyi mtasema hivi: ‘Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.’

14. Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa nyinyi hamtapata matatizo.”

15. Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.

16. Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagizia Yesu.

17. Walipomwona wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka.

18. Yesu akaja karibu, akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

19. Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.

20. Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.”

Kusoma sura kamili Mathayo 28