Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 27:44-55 Biblia Habari Njema (BHN)

44. Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.

45. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote.

46. Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

47. Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.”

48. Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.

49. Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.”

50. Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.

51. Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

52. makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;

53. nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.

54. Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”

55. Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.

Kusoma sura kamili Mathayo 27