Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 26:57-68 Biblia Habari Njema (BHN)

57. Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee.

58. Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa.

59. Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua,

60. lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili,

61. wakasema, “Mtu huyu alisema: ‘Ninaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’”

62. Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?”

63. Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!”

64. Yesu akamwambia, “Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65. Hapo, kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake.

66. Nyinyi mwaonaje?” Wao wakamjibu, “Anastahili kufa!”

67. Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi,

68. wakasema, “Tubashirie basi, wewe Kristo; ni nani amekupiga!”

Kusoma sura kamili Mathayo 26