Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 26:53-63 Biblia Habari Njema (BHN)

53. Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika?

54. Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?”

55. Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata!

56. Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.

57. Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee.

58. Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa.

59. Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua,

60. lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili,

61. wakasema, “Mtu huyu alisema: ‘Ninaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’”

62. Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?”

63. Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!”

Kusoma sura kamili Mathayo 26