Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 26:27-39 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote;

28. maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.

29. Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”

30. Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.

31. Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu wa leo, nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema:‘Nitampiga mchungaji,na kondoo wa kundi watatawanyika.’

32. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya.”

33. Petro akamwambia Yesu, “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe.”

34. Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

35. Petro akamwambia, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.

36. Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.”

37. Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko.

38. Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”

39. Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.”

Kusoma sura kamili Mathayo 26