Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 24:27-42 Biblia Habari Njema (BHN)

27. maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

28. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.

29. “Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.

30. Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.

31. Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.

32. “Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia.

33. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.

34. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.

35. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

36. “Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.

37. Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

38. Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.

39. Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.

40. Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

41. Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

42. Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.

Kusoma sura kamili Mathayo 24