Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 23:4-23 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba.

5. Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao.

6. Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi.

7. Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: ‘Mwalimu.’

8. Lakini nyinyi msiitwe kamwe ‘Mwalimu,’ maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu.

9. Wala msimwite mtu yeyote ‘Baba’ hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu, aliye mbinguni.

10. Wala msiitwe ‘Viongozi,’ maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo.

11. Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu.

12. Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.

13. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Nyinyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie. [

14. Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali.] (Taz Marko 12:40).

15. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko nyinyi wenyewe.

16. “Ole wenu viongozi vipofu! Nyinyi mwasema ati mtu akiapa kwa hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya hekalu, kiapo hicho kinamshika.

17. Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: Dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?

18. Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.

19. Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: Ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?

20. Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake.

21. Na anayeapa kwa hekalu ameapa kwa hilo hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake.

22. Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.

23. Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.

Kusoma sura kamili Mathayo 23