Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 23:17-29 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: Dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?

18. Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.

19. Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: Ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?

20. Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake.

21. Na anayeapa kwa hekalu ameapa kwa hilo hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake.

22. Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.

23. Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.

24. Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia!

25. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyanganyi na uchoyo.

26. Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia.

27. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu.

28. Hali kadhalika nyinyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

29. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema.

Kusoma sura kamili Mathayo 23