Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 20:8-24 Biblia Habari Njema (BHN)

8. “Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, ‘Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.’

9. Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja fedha dinari moja.

10. Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.

11. Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnungunikia yule bwana.

12. Wakasema, ‘Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?’

13. “Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa dinari moja?

14. Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15. Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?’”

16. Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

17. Yesu alipokuwa anakwenda juu Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,

18. “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe.

19. Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.”

20. Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.

21. Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.”

22. Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.”

23. Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.”

24. Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.

Kusoma sura kamili Mathayo 20