Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 2:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: Dhahabu, ubani na manemane.

12. Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.

13. Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.”

14. Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri.

15. Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie:“Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.”

16. Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota.

17. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia:

18. “Sauti imesikika huko Rama,kilio na maombolezo mengi.Raheli anawalilia watoto wake,wala hataki kutulizwa,maana wote wamefariki.”

19. Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri,

20. akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.”

21. Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli.

22. Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya,

Kusoma sura kamili Mathayo 2