Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 19:14-30 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Yesu akasema, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.”

15. Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.

16. Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uhai wa milele?”

17. Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uhai, shika amri.”

18. Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, Usizini, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo,

19. Waheshimu baba yako na mama yako; na, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”

20. Huyo kijana akamwambia, “Hayo yote nimeyazingatia; nifanye nini zaidi?”

21. Yesu akamwambia, “Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako, uwape maskini fedha hiyo, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.”

22. Huyo kijana aliposikia hayo, akaenda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.

23. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.

24. Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

25. Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi, awezaye kuokoka?”

26. Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”

27. Kisha Petro akasema, “Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?”

28. Yesu akawaambia, “Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti chake cha enzi kitukufu katika ulimwengu mpya, nyinyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.

29. Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uhai wa milele.

30. Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Kusoma sura kamili Mathayo 19