Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 14:3-12 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake.

4. Kisa ni kwamba Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!”

5. Herode alitaka kumuua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii.

6. Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa,

7. hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba.

8. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, “Nipe papa hapa katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.”

9. Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe.

10. Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane.

11. Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake.

12. Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.

Kusoma sura kamili Mathayo 14