Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 11:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?

8. Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme.

9. Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.

10. “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu:‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie,ambaye atakutayarishia njia yako’.

11. Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye.

12. Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu.

13. Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi.

14. Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja.

15. Mwenye masikio na asikie!

16. “Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine:

Kusoma sura kamili Mathayo 11