Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 10:24-41 Biblia Habari Njema (BHN)

24. “Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumishi hampiti bwana wake.

25. Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je, hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?

26. “Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa.

27. Ninalowaambieni nyinyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinongonezwa, litangazeni hadharani.

28. Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu.

29. Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu.

30. Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

31. Kwa hiyo msiogope; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi.

32. “Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

33. Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

34. “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga.

35. Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake.

36. Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.

37. “Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili.

39. Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.

40. “Anayewapokea nyinyi, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.

41. Anayempokea nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayempokea mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema.

Kusoma sura kamili Mathayo 10