Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 9:29-43 Biblia Habari Njema (BHN)

29. Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wanaoongea Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua.

30. Wale ndugu walipogundua jambo hilo, walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso.

31. Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu.

32. Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda.

33. Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza.

34. Basi, Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako.” Ainea akaamka mara.

35. Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Ainea, na wote wakamgeukia Bwana.

36. Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima.

37. Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakaulaza katika chumba ghorofani.

38. Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: “Njoo kwetu haraka iwezekanavyo.”

39. Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai.

40. Petro aliwatoa nje wote, akapiga magoti, akasali. Kisha akaigeukia ile maiti, akasema, “Tabitha, amka.” Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro, akaketi.

41. Petro akamsaidia kusimama, halafu akawaita wale watu wa Mungu na wale wajane, akamkabidhi kwao akiwa mzima.

42. Habari za tukio hili zilienea kila mahali huko Yopa, na watu wengi wakamwamini Bwana.

43. Petro alikaa siku kadhaa huko Yopa, akiishi kwa mtu mmoja mtengenezaji wa ngozi aitwaye Simoni.

Kusoma sura kamili Matendo 9