Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 8:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua kuwa sawa.Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria.

2. Watu wamchao Mungu walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa.

3. Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani.

4. Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe.

5. Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo.

6. Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya.

7. Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa.

8. Kukawa na furaha kubwa katika mji ule.

9. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu.

10. Watu wote, wadogo kwa wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, “Simoni ndiye nguvu ya kimungu inayoitwa ‘Nguvu Kubwa.’”

11. Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu.

12. Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume.

13. Hata Simoni aliamini; na baada ya kubatizwa alikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika.

Kusoma sura kamili Matendo 8