Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 7:11-31 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote.

12. Basi, Yakobo aliposikia habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza.

13. Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu.

14. Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na watano, waje Misri.

15. Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa.

16. Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alikuwa amenunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.

17. “Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi.

18. Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza kutawala huko Misri.

19. Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe.

20. Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu,

21. na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea kama mtoto wake.

22. Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo.

23. “Alipokuwa na umri wa miaka arubaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli.

24. Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kwa kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. (

25. Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo).

26. Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’

27. Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?

28. Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’

29. Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.

30. “Miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai.

31. Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:

Kusoma sura kamili Matendo 7