Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 5:34-42 Biblia Habari Njema (BHN)

34. Lakini Mfarisayo mmoja aitwaye Gamalieli ambaye alikuwa mwalimu wa sheria na aliyeheshimika sana mbele ya watu wote, alisimama mbele ya lile Baraza, akataka wale mitume watolewe nje kwa muda mfupi.

35. Kisha akawaambia wale wajumbe wa Baraza, “Wananchi wa Israeli, tahadhari kabla ya kutekeleza hicho mnachotaka kuwatenda watu hawa!

36. Zamani kidogo, kulitokea mtu mmoja jina lake Theuda, akajisema kuwa mtu wa maana na watu karibu 400 wakajiunga naye. Lakini aliuawa, kisha wafuasi wake wote wakatawanyika na kikundi chake kikafa.

37. Tena, baadaye, wakati ule wa kuhesabiwa watu, alitokea Yuda wa Galilaya. Huyu naye aliwavuta watu wakamfuata; lakini naye pia aliuawa, na wafuasi wake wakatawanyika.

38. Na sasa pia mimi nawaambieni, msiwachukulie watu hawa hatua yoyote; waacheni! Kwa maana, ikiwa mpango huu au shughuli yao hii imeanzishwa na binadamu, itatoweka yenyewe.

39. Lakini kama imeanzishwa na Mungu, siyo tu kwamba hamtaweza kuwashinda, bali mtajikuta mnampinga Mungu.”Basi, wakakubaliana naye.

40. Hivyo wakawaita wale mitume, wakaamuru wachapwe viboko na kuwaonya wasifundishe tena kwa jina la Yesu; kisha wakawaacha waende zao.

41. Basi, mitume wakatoka nje ya lile Baraza wakiwa wamejaa furaha, kwani walistahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu.

42. Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo hekaluni na nyumbani kwa watu.

Kusoma sura kamili Matendo 5